NAAM tumekutana tena kwenye kona ya mapenzi na uhusiano ili kujuzana machache yahusuyo mahaba. Kila kukicha kona hii imekuwa msaada mkubwa kwa wapenzi na kurudisha furaha, kujenga ujasiri mioyoni mwa watu na kuokoa penzi lililotaka kuvunjika.
Hii imenifanya niangalie kwa undani matatizo mengi katika maisha yetu ya kila siku hususani mapenzi ambayo ndiyo muhimili wa maisha yetu. Nina matumaini wote mu wazima kwa uwezo wa Manani.
Kama nilivyoeleza jinsi watu walivyoumizwa na mapenzi mwaka uliopita kiasi cha kukata tamaa na kujishusha hadhi na kujiona hawana tena thamani, lakini kupitia mada ya leo ni nafasi nyingine ya kujitambua.
Nimekuwa nikipokea maswali mengi kwa njia ya ujumbe mfupi, lakini napenda kuwaambia wasomaji wa kona ya Mapenzi na Uhusiano mwenye swali linalohitaji majibu apige simu na atajibiwa kwa ufasaha. Kama wengine waliopita na kupata ufumbuzi wa matatizo yao.
Leo tunaendelea na mada yetu kuijua thamani yako.
Swali linakuja thamani yako ni nini?
Thamani yako ni kujijua kuwa wewe ni mwanadamu umeumbwa kama mwingine hivyo una haki zote anazostahili mwanadamu yeyote.
Haki yako ni ipi?
Kupata chochote cha msingi bila kuingiliwa au kupokonywa na mtu. Baada ya kueleza hayo kwa kifupi sasa tuangalie nia na madhumuni ya mada yetu ya leo. Kutokana na maswali mengi niliyoyapata kutoka kwa watu wengi hasa wanawake kuhusu kuachwa na mpenzi bila sababu na kufanya mtu achanganyikiwe na kujiona hana thamani tena mbele ya jamii.
Wapo wanaochanganyikiwa na kupoteza dira au wengine kuchukua jukumu la kukatisha maisha yao.
Ndiyo maana leo nimeonelea tulizungumze hili kwa yeyote aliyefikwa na maswahibu haya, naelewa kabisa kila aachwae bila sababu hubakia njia panda na kushindwa kuelewa afanye nini. Mwingine hufikia hatua ya kujiona ana upungufu ambao huenda ukawa ugonjwa usiopona wa kupoteza wapenzi.
Ni kweli umeachwa bila sababu, nina imani imeelezea mada nyingi siku za nyuma kuhusu sababu za penzi kuvunjika bila sababu. Sitorudia kwa leo.
Leo mada inaongelea imekwisha tokea au mpenzi wako haeleweki, unalazimisha kumpenda asiye kupenda, mateso ya kujitakia. Penzi limevunjika umechanganyikiwa hujui ufanye nini.
Hapa lazima ujue thamani yako ni nini?
Siku zote mtetezi wa nafsi yako ni wewe mwenyewe, elewa kupendwa na aliyekuacha hakukuwa kwa bahati, sawa na daladala ambayo inakuwa ya mwisho ukiteremshwa njiani hupati tena nyingine.
La hasha, hebu jithamini na kujiona una thamani kubwa mbele ya jamii kwa kupenda au kupendwa na mtu yeyote. Usikate tamaa kwa kuona umeachwa basi ndiyo mwisho wa kupenda au kupendwa.
Jiamini kuwa thamani yako si kwa yule aliyekuacha hakuna wengine tena, si kweli, huenda umeachwa na mmoja kuna mia moja walikuwa wakikuhitaji lakini walikuona tayari upo na mtu.
Siku zote mwisho wa penzi la zamani ni mwanzo wa penzi jipya, unapoachwa usikurupuke kutoa maamuzi. Siku zote maamuzi ya hasira huwa na majuto. Wapo wanaodiliki hata kulipa kisasi.
Ufumbuzi wa penzi linapovunjika ni utulivu, kwani ni njia pekee ya kuweza kujipanga upya. Nina imani baada ya utulivu ni muda muafaka wa kujithamini.
Jiamini na kujiona una thamani ya kusimama kwa mtu yeyote na kujiona thamani yako ambayo ipo toka ulipozaliwa tumboni kwa mama yako. Usijishushe thamani, simama wewe kama wewe na kujiona ni mshindi, kuachwa ona kama ajali ambayo haiepukiki na siku zote ajali haiwezi kukufanya usisafiri tena.
Namalizia kwa kusema, unapojithamini siku zote hakuna kiumbe cha kukubabaisha, siku zote usijishushe kwa vile thamani yako unayeijua ni wewe, unapoumizwa na kitu hakuna mwingine apatae maumivu ila wewe mwenyewe.
Utakaposimama wewe mwenyewe na kuonyesha hubabaishwi na kitu, siku zote wewe ndiye huwa mshindi.
Kwa hayo machache tukutane wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment